Habari ya kuondolewa kwa wimbo wa
Madee ‘Tema Mate’ kwenye kinyang’anyiro cha KTMAs bila shaka zimewasikitisha
wanafamilia wa Tip Top Connection na mashabiki walioipendekeza kwa kura nyingi
ngoma hiyo.
Kwa upande wa Madee amesema kuwa
BASATA wamechelewa katika kuchukua uamuzi huo kwa kuwa wimbo ulitoka zamani na
kushika nafasi ya kwanza kwenye chart nyingi za radio.
“Mimi nahisi walikuwa wamechelewa ndio maana
kila siku nalilia kwamba kuwe kuna chombo ambacho muziki wetu tukishamaliza
kuutengeneza tunapitisha pale then wanasikiliza kama inafaaa kwenda hewani
inafaa kama haifai tunaaambiwa mapema. Lakini chombo hicho hakuna, kwa hiyo
wanakuwa kama wanafake kwa sababu mwisho wa siku wimbo unakuwa unasambaa na
watu wanakuwa wameshaipenda.” Amesema Madee.
Ameeleza kuwa kutokana na kuchelewa
huko watangazaji wa radio na Television ambao wanakuwa wanacheza wimbo huo na
kuuweka kwenye chart kama namba moja, pale unapozuiwa nao wanaonekana kama
hawana maadili bora.
Rapper huyo wa Manzese ameeleza
kuwa hafahamu hasa kwa nini wimbo huo umeonekana hauna maadili wakati yeye
alijua mara ya kwanza kuwa video ya wimbo huo ndiyo iliyokuwa imetajwa kuwa
kinyume na maadili.
Hata hivyo, Madee amesema tangu
aanze muziki miaka 14 iliyopita hajawahi kupata tuzo ya Kili hivyo haoni hasara
yoyote kwa kuondolewa kwenye kinyanyiro hicho.
“Nimeshazoea yaani haitoniaffect
chochote na wala haitakuwa na hasara yoyote kwenye muziki wangu, zaidi tu ni
kuwashukuru wale ambao walisapoti muziki wangu ukafika huko mpaka watu wakakaa leo
kuijadili, wamepoteza dakika zao kadhaa kuijadili kwa hiyo ni kawaida mimi
sioni kama nitaathirika na chochote.” Madee ameongeza.
Tovuti ya Times Fm ilimtafuta kaimu
katibu mtendaji wa BASATA, Godfrey Mnengereza na kumuuliza mtazamo wake na
BASATA kuhusu alichokisema Madee.
“Nimependa sana maoni ya Madee,
kumbe tuko pamoja kwamba hazungumzii kwamba wimbo wake haukidhi hivyo vigezo.
Anazungumzia na anatoa ushauri kwa baraza kwamba tumechelewa kwa sababu wimbo
umepigwa mwaka mzima na kwamba tufanye censorship. Kwa sasa hivi ni kweli
ninakubali kabisa kwamba si sahihi sana wimbo uende hewani ndipo tuanze
kuzuia.” Amesema Godfrey Mnengereza.
“Kwa upande wa tuzo mchakato wake
ndio umeenza sasa na tunaangalia kazi zilizopita. Lakini nimeshukuru sana kwa
ushauri wake kwamba tuweze kufanya censorship, na ndiko tunakoelekea kwamba
katika suala zima la urasimishaji kazi yoyote ya muziki wa audio inabidi ipite
baraza, sasa ni kwamba tu ni kitu bado kigeni. Lakini vile vile tunatakiwa
tushirikiane na vyombo vya habari kwamba wasiruhusu kazi ambazo zinamdhalilisha
msanii mwenyewe, au zina matusi ndani yake au zina lugha ya uchochezi.” Kaimu
Katibu mtendaji wa BASATA ameileza tovuti ya Times Fm.
Mbali na wimbo wa Madee ‘Tema
Mate’, nyimbo nyingine zilizoondolewa kwenye KTMAs kwa madai ya kukiuka maadili
ni Uzuri Wako ya Jux, na Nimevugwa ya Snura
No comments:
Post a Comment