Kundi la wanamgambo wa kiisilamu la Al shabaab nchini
Somalia limedai kutekeleza mauaji ya watu zaidi ya thelathini nchini Kenya kwa
mujibu wa taarifa za vyombo vya habari nchini Kenya ( Citizen TV) na pia kupitia
kwa ukurasa wake wa Twitter.
Shirika la habari la Reuters pia limesema kuwa Al Shabaab
linasema kwamba Kenya ilipuuza mara kwa mara vitisho vya kundi hilo
kuishambulia.
Taarifa kutoka Ikulu ya Rais Kenya zinasema kuwa mshukiwa
mmoja amekamatwa. Mshukiwa huyo amejeruhiwa na anapokea matibabu hospitalini.
Wanamgambo wa Al Shabaab wanasema kuwa Kenya haikuchukulia
kwa uzito onyo walilotoa kwa taifa hilo kwa hatua ya kuwapeleka wanajeshi wake
nchini humo kupambana dhidi yao.
Kundi hilo limesema limekuwa likitoa onyo mara kwa mara kwa
Kenya kuwa ikiwa haitaondoa vikosi vyake nchini Somalia, athari zitakuwa mbaya
mno.
Kupitia mtandao wao wa Twitter, Al Shabaab limesema kuwa Kenya
ilijidai kutosikia onyo hizo, na kuendelea kuwaua waisilamu wasio na hatia
nchini Somalia.
Taarifa hiyo ya Twitter ilisema kuwa Shambulio la Westgate
ni tone katika bahari tu ya mfano wa yanayowakumba wasomali waisilamu nchini
Somalia.
Taharuki ilianza hii leo saa saba mchana wakati watu
wanaokisiwa kuwa kumi walipovamia jengo la kifahari la Westgate la kuwapiga
risasi kiholela wakenya waliokuwa wanaendelea na shughuli zao za kawaida.
Kwa mujibu wa shirika la msalaba mwekundu , takriban watu 30
walifariki kwa kupigwa risasi au kutokana na majeraha yao na wengine wengi
wenye majeraha ya risasi kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.
No comments:
Post a Comment